Featured
Showing posts with label sport. Show all posts
Showing posts with label sport. Show all posts

Thursday, September 22, 2016

DIAMOND TRUST BANK YADHAMINI LIGI KUU YA VODACOM




Benki ya Diamond Trust (DTB) leo imesaini kuingia mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kudhamini Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (VPL) kwa msimu wa mwaka 2016/2017.
DTB inaungana na mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na wadhamini wengine katika kudhamini ligi hiyo maarufu kama Ligi Kuu ya Vodacom.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya utiaji saini huo iliyofanyika Hoteli ya Serena, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Benki hiyo, Joseph Mabusi amesema:  “Udhamini huu utasaidia zaidi maendeleo ya soka nchini kwa kuziwezesha timu timu shiriki pamoja na jitihada zingine za TFF. Soka inaunganisha Watanzania wa matabaka mbalimbali ambao ni wateja wetu na si kama benki tungependa kuwa karibu nao zaidi kupitia mchezo huu.”
Mabusi aliongeza kwa kusema:  “Tunafurahi na kujivunia kuwa sehemu ya ligi kuu na tunaamini udhamini huu utazidisha ari ya kuwahudumia Watanzania wote.
Benki ya Diamond Trust imekuwa ikiipa kipaumbele michezo mbalimbali ikiwemo soka, ambapo timu rasmi ya soka inayoundwa na Wafanyakazi imefanikiwa kushinda vikombe na mataji mbalimbali ya soka likiwemo taji la ligi ya mabenki nchini inayojulikana kama BRAZUKA KIBENKI mwaka 2015 pamoja na ngao ya hisani ya ligi hiyo mwaka 2016.
Benki pia inadhamini timu ya soka ya Agathon iliyopo Mbagala inayoshiriki ligi soka daraja la tatu. Zaidi ya hayo benki pia inajivunia kuwa moja kati ya wadhamini wa michuano ya CECAFA Kagame Cup mwaka 2015.
Ligi hiyo inajumuisha timu 16 kutoka Tanzania bara zinazocheza kwa mfumo wa mechi za nyumbani na ugenini ambazo ni Young Africans, Simba Sports Club, Azam FC, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Mbeya City, Majimaji, MbaoFC, African Lyon, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Tanzania Prisons, Stand United, mwadui FC, Ndanda FC na Toto Africans.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Shirikisho la Soka Tanznaia –TFF wakiongozwa na Rais wao Ndugu Jamal Malinzi, Wafanyakazi wa Benki ya DTB, wawakilishi kutoka Vodacom, wadau mbalimbali wa soka pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Malinzi ameshukuru na kuupongeza udhamini huo uliotolewa na benki hiyo na pia ameziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo ili kukuza soka nchini. “Kwa heshima ana furaha kubwa nawakaribisha DTB Tanzania kwenye ligi kuu na familia ya TFF kwa ujumla.”
Benki ya Diamond Trust ina matawi 25 nchini, ikiwa na matawi kumi na moja (11) jijini Dar es Salaam (Mtaawa Jamaat, Masaki, Morocco, Magomeni, Mbezi, Mbagala, barabara ya Nyerere, Msimbazi - Kariakoo, barabara ya Nelson Mandela, Upanga katika barabara ya umoja wa mataifa na katika makutano ya barabara ya Mirambo na mtaa wa Samora).
Vile vile ina matawi katika miji ya Arusha (2), Mwanza (2) na katika miji ya Dodoma, Kahama, Mbeya, Morogoro, Moshi, Mtwara, Mwanza, Tabora ,Tanga na Zanzibar.
DTB Tanzania ni mshirika wa mtandao wa maendeleo ya kiuchumi wa Aga Khan - Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) ambao ni sehemu ya mtandao wa maendeleowa Aga Khan Development Network).

DTB Kenya ni miongoni mwa wanahisa muhimu wa DTB Tanzania.

Mabadiliko ya Ratiba Ligi Kuu VPL





Mechi mbili za raundi ya sita za Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Majimaji, na African Lyon na Kagera Sugar sasa zitachezwa kwenye Uwanja wa Taifa badala ya Uwanja wa Uhuru.
Mabadiliko hayo yametokana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusitisha kwa muda kuutumia Uwanja wa Uhuru katika kipindi hiki ambacho limeanza kufanyia marekebisho sehemu ya uwanja huo ambayo ni ya nyasi bandia (artificial turf).

Hivyo, mechi ya Simba na Majimaji itafanyika Jumamosi, Septemba 24 wakati ile ya African Lyon na Kagera Sugar itachezwa Jumatatu, Septemba 26. Jumapili, Septemba 25 Uwanja Taifa utatumiwa kwa mechi ya timu za Wabunge za Simba na Yanga ili kuchangia waathirika wa janga la tetemeko lililotokea mkoani Kagera.
Mechi nyingine za Ligi Kuu ya Vodacom zitakazochezwa Jumamosi, Septemba 24 ni kati ya JKT Ruvu na Mbeya City (Mabatini), Ndanda na Azam (Nangwanda Sijaona), Tanzania Prisons na Mwadui (Sokoine), Mtibwa Sugar na Mbao (Manungu).
Jumapili kutakuwa na mechi kati ya Stand United na Yanga (Kambarage), na Ruvu Shooting na Toto Africans kwenye Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.

Kutokana na marekebisho yanayofanyika Uwanja wa Uhuru, mechi ya kundi ya A ya Ligi Daraja la Kwanza kati ya Ashanti United na Pamba iliyokuwa ichezwe Ijumaa, Septemba 23 kwenye uwanja huo sasa itafanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

Thursday, September 8, 2016

SERENGETI BOYS YAENDA SHELISHELI


Kikosi cha nyota 21 wa timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, kimeondoka jana alfajiri Septemba 5, 2016 kwa kwenda jijini Victoria, kwenye Kisiwa cha Mahe nchini Shelisheli kwa ajili ya kupiga kambi kujiandaa na mchezo dhidi ya Congo-Brazzaville utakaofanyika Septemba 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Serengeti Boys itacheza na Congo-Brazzaville katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17. Fainali za vijana zitafanyika mwakani nchini Madagascar.
Itakumbukwa kwamba Benchi la ufundi lilimshauri Rais wa TFF, Jamal Malinzi kwamba kambi hiyo ipigwe Shelisheli. Hii ni mara ya pili kwa Malinzi kutimiza ahadi yake kwa wachezaji hao. Kwa mara ya kwanza aliahidi kuwapa kambi ya nje kama wangewatoa Shelisheli.

Timu kweli ilikwenda Madagascar kabla ya kuivaa Afrika Kusini ‘Amajimbos’ na kuitoa na kwa sasa inakwenda Shelisheli kujipanga kwa ajili ya kuitoa Congo-Brazzaville katika harakati za kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.

Monday, September 5, 2016

AZAM FC YATUA SALAMA JIJINI MBEYA KUKABILIANA NA MBEYA CITY



 BAADA ya safari ndefu ya takribani saa 16, hatimaye kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kimewasili salama jijini Mbeya saa 2 usiku huu kikiwa na morali kubwa ya kuibuka ushindi kwenye mechi zake mbili mkoani hapa.
Azam FC imetua mkoani humu kwa malengo ya kubeba pointi sita kwenye mechi zake za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Tanzania Prisons (Septemba 7) na Mbeya City (Septemba 10), zitakazofanyika Uwanja wa Sokoine.
Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez na wasaidizi wake Yeray Romero (Kocha Msaidizi), Pablo Borges (Kocha Msaidizi wa Viungo), Jose Garcia (Kocha wa Makipa), Sergio Perez (Mtaalamu wa Tiba za Viungo) na Martine Valentine (Daktari), wameondoka na nyota wote wa kikosi hicho.
Nyota hao waliowasili hapa ni Kipa Mwadini Ally, mabeki Aggrey Morris, Pascal Wawa, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Ismail Gambo, Gadiel Michael, viungo Frank Domayo, Michael Bolou, Mudathir Yahya, Abdallah Masoud, Ramadhan Singano, Khamis Mcha pamoja na washambuliaji Francisco Zekumbawira na Gonazo Bi Thomas.
Wachezaji wengine waliokuwa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Aishi Manula, David Mwantika, Himid Mao, John Bocco na Jean Mugiraneza aliyeko Rwanda 'Amavubi, hao wanatarajia kutua mkoani hapa kesho Jumatatu asubuhi kwa usafiri wa ndege.
Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji chenye ladha safi inayochangamsha mwili Azam Cola, kikiwa mkoani hapa kimeweka kambi yake katika Hoteli ya Manyanya yenye utulivu mkubwa.

JE NGASA KUTUA BONGO ATARUHUSIWA KUSAJILIWA IKIWA DIRISHA LA USAJILI LIMEFUNGWA?





Baada ya Mrisho Ngasa kukanyaga ardhi ya Tanzania maswali kwa wadau wa soka yamekuwa ni kutaka kujua kama mchezaji huyo wa zamani wa Yanga ataruhusiwa kujiunga na klabu yoyote itakayomuhitaji.
Sports Extra ya Clouds ilimtafuta afisa habari wa TFF Alfred Lucas ili kujua taratibu na kanuni zikoje endapo kama kuna timu itataka kumsajili Ngasa kwa ajili ya michuano ya ligi kuu Tanzania bara lakini hata ikibidi mashindano ya kimataifa.

Lucas amesema Ngasa ananafasi ya kujiunga na timu yeyote itakayomuhitaji huku usajili huo ukitakiwa kufanywa kabla ya Septembre 6.
“Hata sisi tumeiona taarifa ya Ngasa kuwa hana mkataba tena na Free State Stars sasa kwa usajili wetu wa hapa nyumbani anaweza akapata nafasi kwasababu dirisha la usajili la FIFA linafungwa September 6 na hii lazima ieleweke vizuri sana, kilichofanya Yanga achelewe wakati ule ni usajili wa ndani kwa maana ya kwamba sisi TFF tulifungua usajili wa ndani kuanzia 15 June -16 August lakini kwa upande wa kimataifa dirisha linafungwa September 6”, Alfred Lucas alikaririwa na Clouds FM kupitia Sports Extra.
“Kwahiyo kama itatokea timu inamtaka kwasababu kama ameshapewa barua ya kuachwa kwaiyo inaweza ikamlinda kufdanyiwa  usajili.”
Ngasa amerejea Tanzania September 3 akitokea South Africa ambapo alivunja mkataba wake na klabu ya Free State Stars inayoshiriki ligi kuu nchini humo.

Baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa jijini Dar, Ngasa hakuwa tayari kuzungumza lolote juu ya kuvunja mkataba na kurejea nyumbai badala yake akasema: “Nimerudi nyumbani kwa sasa imi ni mchezaji huru nimekuja kupumzika kidogo kisha nitasema nitaenda kucheza wapi.”

Monday, August 29, 2016

Asamoah Gyan arudi Uingereza


Nahodha wa kikosi cha soka nchini Ghana Asamoah Gyan anatarajiwa kujiunga na klabu ya Reading kwa mkopo kutoka timu ya China Shanghai SIPG.
Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Sunderland anafanyiwa ukaguzi wa matibabu na klabu hiyo ya daraja la kwanza.
Gyan aliifungia mabao 30 Sunderland alipoichezea timu hiyo kwa misimu miwili,kutoka mwaka 2010 kabla ya kuelekea Al-Ain ya Umoja wa Milki za kiarabu UAE.
Alijiunga na Shanghai 2015 wakati huo na alikuwa miongoni mwa mchezaji wanaolipwa zaidi duniani. 

Kocha Azam FC aridhishwa na vipaji Temeke, sasa zamu ya U-17 Ilala Jumamosi ijayo


MKUU wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, ameridhishwa na viwango vya wachezaji vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17) kutoka Wilaya ya Temeke na Kigamboni waliojitokeza kwenye majaribio yaliyofanyika jana Jumapili ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Azam FC imeanza mchakato rasmi wa kuunda kizazi kipya cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, mpango ambao itazunguka mikoa 13 nchi nzima, ambapo kwa kuanzia tayari imefanikiwa kumaliza majaribio ndani ya eneo la Wilaya ya Temeke na Kigamboni, wakijitokeza vijana 423 na kuchaguliwa watano tu.
Legg ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc kuwa mara baada ya zoezi hilo kukamilika kwa mafanikio makubwa kwenye maeneo hayo mawili, hivi sasa amewakaribisha vijana wa umri huo kutoka Wilaya ya Ilala watakaotakiwa kujitokeza kwa wingi ndani ya Uwanja wa Jakaya Kikwete Park (JMK Park) Jumamosi ijayo Septemba 3 mwaka huu.
Vijana hao watatakiwa kufika kwa ajili ya majaribio hayo kuanzia saa 1.00 asubuhi wakiwa na vyeti vyao vya kuzaliwa na wazazi au walezi wao, ambao watawaongoza na kuwashuhudia wanapoonyesha viwango vyao pamoja na kutoa msaada wowote wa kumwelezea kijana wake pale itakapohitajika.
“Kulikuwa na viwango vizuri leo (jana), tulitarajia kupokea vijana zaidi takribani 500 hapa lakini wamejitokeza 423, lakini tunaamini tutapata vijana zaidi kwa majaribio ya pili Wilaya ya Ilala ndani ya JMK Jumamosi ijayo.
“Viwango vilikuwa vizuri, hususani dakika 45 za mwisho kwenye mechi iliyohusisha vijana 23 tuliowachagua hadi mchujo wa mwisho na hatimaye kupata watano wa mwisho, hatukuweza kuchagua wengi zaidi kwa kuwa tunachagua vijana bora zaidi Tanzania nzima, lakini tumeshuhudia viwango vizuri sana,” alisema.

MCHEZO WA LIGI KUU YOUNG AFRICANS V JKT RUVU



Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imethibitisha kuwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na JKT Ruvu ya Pwani, ulipangwa kufanyika Jumatano Agosti 31, 2016 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam imeahirishwa mpaka itakapopangiwa tarehe nyingine.

Mechi hiyo imeondolewa kutokana na timu ya Young Africans kuwa na wachezaji wengi kwenye kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) kinachosafiri Agosti 31, 2016 asubuhi kwenda Lagos, Nigeria kwa ajili ya mechi ya mchujo ya michuano ya Kombe la Afrika (AFCON Qualifiers) itakayochezwa Septemba 3, 2016.
Mabadiliko hayo hayatavuruga ratiba ya mechi zinazofuata za Ligi Kuu ya Vodacom kwa timu husika.

Tayari wahusika wakiwamo Young Africans na JKT Ruvu SC, wamejulishwa.

Saturday, August 27, 2016

MWANGALIE SAMATTA NDANI YA KUNDI F UROPA LEAGUE





Baada ya jana Mbwana Samatta kuisaidia Genk kufuzu hatua ya makundi ya Europa League, leo tayari makundi yamepangwa huku Genk ikiwa katika Kundi F pamoja na timu za Athletic Bilbao, Rapid Vienna na Sassuolo .
Makundi yote yapo kama ifuatavyo…

UEFA YAFANYA MABADILIKO CHAMPIONS LEAGUE




Shirikisho la soka la Ulaya UEFA limetangaza mabadiliko katika michuano ya UEFA Champions League kuanzia msimu ujao 2017-18.
Kuanzia msimu ujao, timu 4 za juu kutoka katika ligi 4 bora barani Ulaya (La Liga, Premier League, Budesilga na Serie A) zitakuwa zinafuzu moja kwa moja kuingia hatua ya makundi bila kupitia hatua ya mtoano.

Awali timu zilizoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hizo zilikuwa zinacheza mchezo wa mtoano (play off) na mshindi ndiyo anafuzu hatua ya makundi kama ilivyofanyika pia katika msimu huu.

KIKOSI CHA TAIFA STARS YA KUIVAA NIGERIA HIKI HAPA




Kocha Mkuu wa timu ya Mpira wa Miguu Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, ametangaza wachezaji 20 watakaounda kikosi kitakachosafiri mwishoni mwa mwezi huu kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017) dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles.
Licha ya mchezo huo wa Septemba 3, 2016 kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon, lakini utakuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo iliyojitoa katikati ya mashindano.

“Tanzania hatuwezi kupuumza mchezo huu, tumeuchukulia serious (kwa umakini) kabisa kwa sababu tunacheza ugenini ambako matokeo mazuri yanaweza kutusongesha mbele na kuingia ndani ya timu 99 bora katika viwango vya FIFA,” amesema Mkwasa.
Katika kikosi chake, Mkwasa ametangaza kutomjumuisha Mshambuliaji wa Kimataifa, Thomas Ulimwengu anayecheza klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutokana na majeruhi ya paja kama ilivyo kwa Juma Abdul wa Young Africans ambaye aliumia katika mchezo wa kuwania Kombe la Shirikisho dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria.
“Timu itaingia kambini Agosti 28, itakaa kambini kwa siku tano kabla ya kusafiri kucheza mchezo huo wa kukamilisha ratiba ambao Misri tayari wameshafuzu fainali za Afrika,” amesema Mkwasa na kuongeza kuwa kuna mchezaji wa Tanzania, Said Carte Mhando anamfuatilia ili ikiwezekana baadaye amwite kuchezea timu ya taifa. Anakipiga Klabu ya Brencia Calcio ya Italia.

Wachezaji walioitwa:
Makipa-
Deogratius Munishi – Young Africans
Aishi Manula – Azam FC

Mabeki
Kelvin Yondani - Young Africans
Vicent Andrew - Young Africans
Mwinyi Haji - Young Africans
Mohamed Hussein – Simba SC
Shomari Kapombe - Azam FC
David Mwantika - Azam FC

Viungo
Himid Mao - Azam FC
Shiza Kichuya – Simba SC
Ibrahim Jeba – Mtibwa Sugar
Jonas Mkude – Simba SC
Muzamiru Yassin – Simba SC
Juma Mahadhi - Young Africans
Farid Mussa Tenerif ya Hispania

Washambuliaji
Simon Msuva - Young Africans
Jamal Mnyate – Simba SC
Ibrahim Ajib – Simba SC
John Bocco - Azam FC


Mbwana Samatta - CK Genk ya Ubelgiji

Tuesday, August 23, 2016

TFF YATOA TAHADHARI KWA TIMU TANO VPL....



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linapenda kutoa tahadhali kwa timu tano za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) juu ya kuwatumia wachezaji ambao imewasajili, lakini imebainika mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kwamba wanamatatizo kwenye usajili wao.


Majimaji ya Songea
Mchezaji anayefahamika kwa majina ya George Mpole ambaye pia amebainika kuwa ndiye Gerald Mpole wa Majimaji ya Songea amefungiwa kucheza soka kwa mwaka kwa kosa la kubadili jina akiwa na lengo la kufanya udanganyifu kwenye usajili. Majimaji imeagizwa kutomtumia mchezaji huyo kutoka Kimondo FC.
Mwadui FC ya Shinyanga
Mchezaji William Lucian aliyesajiliwa na Mwadui ya Shinyanga kutoka Ndanda ya Mtwara, naye amefungiwa mwaka mmoja kwa kosa la kusajili Mwadui FC ilihali akiwa hajamaliza mkataba na Ndanda. Mwadui isimtumie mchezaji huyo.
Mbeya City ya Mbeya
Mchezaji Saidi Mkopi, pia amefungiwa mwaka mmoja kwa kosa la kujisali timu mbili. Imebainika kuwa akiwa bado na mkataba na Tanzania Prisons ya Mbeya hivyo Mbeya City isi1mtumie mchezaji huyo.
African Lyon ya Dar es Salaam
Mchezaji Rehani Kibingu aliyesajiliwa na African Lyon ya Dar es Salaam, amesimamishwa kuchezea timu hiyo mpaka uongozi wa African Lyon kumalizana na Ashanti United ya Dar es Salaam kabla ya Agosti 27, 2016. African Lyon isimtumie mchezaji huyo kwa sasa.
Mbao FC ya Mwanza


Mchezaji Emmanuel Kichiba aliyesajiliwa Mbao FC, naye amesimamishwa mpaka Mbao watakapomalizana na Ashanti United ya Dar es Salaam, kabla ya Agosti 27, 2016. Mbao FC isimtumie mchezaji huyo kwa sasa.

FIFA YAONGEZEA UJUZI MAKOCHA TANZANIA

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwa mara nyingine limeipa nafasi Tanzania kwa kutoa kozi maalumu ya stamina (Physical fitness) kwa makocha wa Tanzania wenye leseni kiwango B inayoanza leo Agosti 22, 2016. Kozi hiyo inayoendeshwa na mkufunzi kutoka FIFA, Dk. Praddit Dutta, raia wa India itafikia ukomo Ijumaa wiki hii.
Akifungua kozi hiyo, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine aliishukuru FIFA kwa namna inavyoipa nafasi Tanzania katika kozi mbalimbali hususani za ukocha na uamuzi.

“Si kila nchi inapata privilege (fursa) kama hii. Bila shaka FIFA inatambua uwezo wa makocha wa Tanzania kwa sasa. Mjue kuwa FIFA ina watu wa kuwapa taarifa kila kona. Kama mngekuwa mnafanya vibaya, FIFA wangesema Tanzania bado, kwa hiyo kozi zisipelekwe… lakini inaonekana mnafanya vema, mngefanya vibaya msingefikiriwa,” alisema Mwesigwa aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo.
Mwesigwa amesema kwa kuwa FIFA ina malengo chanya na Tanzania kwa kutoa kozi mbalimbali ikiwamo hiyo ya physical fitness inayolenga kuwapa ujuzi makocha hao kuwajengea uwezo wachezaji kuwa na stamina.
Hivyo akawataka makocha wanaohudhuria kozi hiyo kutumia fursa hiyo ya mafunzo si kwa ajili yao peke yao bali kuendeleza ujuzi huo kwa wengine ambao hawakubahatika kuwa sehemu ya wateule wa FIFA.
Naye, Mkufunzi wa kozi hiyo, Dk. Dutta alisema: “Bila shaka Tanzania inakwenda kufungua ukurasa mwingine wa soka la weledi kwa kuwa na wataalamu mbalimbali katika ukocha na uamuzi. Mnachotakiwa ni kujitahidi kufanya vema na kozi nyingine nyingi zinakuja.”
FIFA kwa kushirikiana na Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Mkurugenzi Salum Madadi, imepitisha majina ya makocha 27 kuhudhuria kozi hiyo inayofanyika katika Hosteli ya TFF iliyoko kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Makocha wanashiriki kozi hiyo ni Mohammed Muza, Samwel Moja, Nassa Mohammed, Jemedari Said, Oscar Mirambo, Wane Mkisi, Cletus Mutauyawa, Shaweji Nawanda, Kizito Mbano, Dennis Kitambi, Sebastian Nkoma, Fikiri Mahiza, Nyamtimba Muga, Nassor Mwinchui, Alfred Itaeli, Henry Ngondo, John Tamba, Kidao Wilfred, Luhaga Makunja, Mohammed Tajdin, Mohammed Silima, Salum Ali Haji, James Joseph, Kessy Mziray, Daudi Sichinga, Bakari Shime na Salum Mayanga.

Monday, August 22, 2016

Kocha wa Azam FcZeben aomba muda zaidi, kurekebisha makosa vs Majimaji




KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amesema kuwa anahitaji muda zaidi ili kukisuka kikosi chake na kucheza kupitia mifumo wanayoendelea kuwafundisha wachezaji wa timu hiyo.
Zeben pia ametanabaisha kuwa atayafanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Lyon ulioisha kwa sare ya 1-1, ili waweze kufanya vizuri mchezo ujao dhidi ya Majimaji.
“Kwa sasa tunafanya tathimini ya mchezo uliopita, kutoa makosa na kurekebishana pale tulipokosea, tukimaliza hapo kwa wiki hii tutaanza kujipanga kwa mchezo ujao (Majimaji), lakini cha kwanza tunaangalia yali yaliyotokea katika mchezo wa kwanza, mapungufu yalikuwa wapi na nani anapaswa kufanya nini,” alisema
Azam FC kwa sasa ni miongoni mwa timu zilizoko nafasi ya nne hadi ya tisa kwenye msimamo wa ligi, zote zikiwa zimekusanyia pointi moja kila mmoja zikizidiwa pointi mbili na vinara Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons, walijikusanyia pointi tatu.
Mechi vs Lyon
Akizungumzia mchezo wa kwanza dhidi ya African Lyon, Zeben alisema timu yake haikucheza vibaya sana kulingana na mechi zilizopita huku akidai kuwa tatizo kubwa linalokikabili kikosi chake ni ufungaji wa mabao.
“Hilo si tatizo sana kadiri muda utakavyokuwa ukienda, hali itabadilika, ni jambo la kuvuta subira na muda zaidi, ukipatikana muda wa kutosha basi timu itakuwa vizuri zaidi mpaka sehemu ya ushambuliaji,” alisema.
Mbali na hilo amesema kuwa wiki hii, atalifanyia kazi suala la wachezaji wake kushindwa kumaliza mechi kipindi cha kwanza, akidai kuwa kwa mechi kadhaa zilizopita kikosi chake kimekuwa kikitafuta ushindi kipindi cha pili kuliko mwanzoni mwa mechi.
“Sikuwa na timu mwanzo, nimeingia kikosini hivi sasa na nimeanza kubadilisha mfumo na mbinu kwa timu kucheza namna tunavyotaka sisi kulingana na mifumo, hilo ni tatizo ambalo lipo ni kubwa kwa sasa na tunaendelea kujitahidi kulifanyia kazi na hata wiki hii tutaendelea nalo ili kwa mechi zijazo liweze kuondoka,” alisema.

Azam FC inakamiwa
Zeben aliendelea kusema kuwa jambo linaloonekana hivi sasa ni timu zote zinazokuja Azam Complex kucheza na timu yake, hufanya jitihada kubwa kuliko uwezo wao ili kuonyesha nao wanaweza kucheza mpira.
“Hili si tatizo kubwa sana inabidi tuendelee kulizoea na nitaendelea kuiboresha timu, ili kwa yoyote atakayekuja Chamazi au nje ya Chamazi tuweze kumfunga,” alisema.
Ligi itakuwa ngumu
Kocha huyo wa zamani wa Stanta Ursula ya Hispania, alisema ameshuhudia mechi za kwanza za ligi msimu huu na kudai kuwa haitakuwa ligi rahisi sana na ngumu kwake yeye kutokana na kikosi alichonacho.
“Cha muhimu ni wachezaji kuendelea kushika mifumo yangu ninayoendelea kuwafundisha, kwa uzoefu wetu tuliokuwa nao hapa tumegundua timu yoyote inayocheza na Azam hata timu iwe kibonde vipi, basi itajitahidi kuweza kuweka rekodi, hili si tatizo sana tutaendele kupambana nalo kwa kuwa hii ni kazi yetu,” alisema.
Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, kitaanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Majimaji kesho Jumanne asubuhi, mechi itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, Jumamosi ijayo saa 10.00 jioni.

SAMATTA AKIZIDI KUTAMBA MBELE YA WAGENI



Mbwana Samatta ameendelea kufanya vyemma kwenye ligi ya Ubelgiji baada ya kufunga magoli magoli mawili wakati Genk ikishinda ugenini kwa magoli 3-0 dhidi ya Lokeren.
Samatta alianza kufunga goli la kwanza dakika ya 34 kipindi cha kwanza kabla ya kufunga bao jingine dakika nne baadaye.
Bao la tatu la Genk limefungwa na Leon Bailey dakika ya 48 kipindi cha pili na magoli hayo yakidumu kwa dakika zote.
Samatta alipumzishwa dakika ya 73 kumpisha mshambuliaji mwenye ya Ugiriki Nikos Karelis.

Huupa chini msimamo wa ligi ya Ubelgiji (Belgium Pro League) ikionesha Genk ikikamata nafasi ya nne kikiwa na pointi saba baada ya kucheza michezo minne.

SERENGETI BOYS YAZIDI KULETA MATUMAINI YA KUELEKEA MADAGASCAR




Timu ya taifa ya vijana chini miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imepata ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya timu ya vijana ya Afrika Kusuni katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex kuwania kufuzu fainali za matifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo mashindano yanayotarajiwa kufanyika Madagascar.
Magoli ya Serengeti Boys yamefungwa na kipindi Mohamed Abdala aliyefunga dakika ya 34 kipindi cha kwanza wakati bao la pili likifungwa dakika za lala salama na Muhsin Makame.
Serengeti Boys imeitupa nje timu ya taifa ya Afrika Kusini kwa jumla ya magoli 3-1 hiyo ni baada ya timu hizo kutoka sare ya kufungana 1-1 kwenye mchezo wa awali uliopigwa Afrika Kusini.

Matokeo hayo yanaifanya Serengeti Boys isonge mbele, itakutana na Namibia au Congo Brazzaville katika raundi inayofuata na endapo itafanikiwa kufuzu basi itakata tiketi ya kushiki katika fainali za mataifa ya Afrika.
Ally Ng’anzi wa Serengeti Boys alioneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo huo baada ya kuoneshwa kadi mbili za njano hivyo ataukosa mchezo mmoja ujao wa timu yake.

September mwaka huu Serengeti itakuwa mwenyeji wa Namibia au Congo Brazzaville huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kuwa kupigwa mwezi October.

Tuesday, August 16, 2016

MASHABIKI KUZOMEA BAADA YA FILIMBI YA MWISHO




Thierry Henry amewatetea washabiki wa Arsenal ambao walizomea timu yao baada ya mchezo dhidi ya Liverpool kumalizika.
Arsenal wamepoteza kwa mabao 4-3 dhidi ya Liverpool baada ya kuruhusu mabao manne ya haraka chini ya dakika 20.
Na mwamauzi wa mchezo huo Michael Oliver alilpopuliza filimbi ya mwisho tu, washabiki wote waligeuka na kuanza kuzomea timu yao.
Arsenal wameshinda mara moja tu michezo ya ufunguzi wa ligi ya England tangu kuingia kwa muongo mpya, na sasa washabiki wa klabu hiyo wanazidi kukatishwa tamaa.
“Washabiki hawakuwazomea wakati wako nyuma kwa 4-1, waliisapoti timu,” alisema Henry kwenye runinga ya Sky Sports. “Lakini baada ya mchezo walikereka na ndiyo maana walizomea.

“Kuna vitu vingi sana vya kuangalia, lakini kikubwa zaidi ni kupoteza nyumbani kwa mara nyingine tena.”

Jamie Redknapp aliongeza: “Sina huruma na Wenger hata kidogo, nadhani vijana wamefanya vyema lakini hawakupaswa kuchezeshwa kwenye mchezo kama ule.
“Unaweza kumpa Giroud dakika 10, Koscielny pia…naamini Payet atacheza kwa upande wa West Ham kesho (leo) .”

Friday, August 12, 2016

Olimpiki Rio: Kocha wa Kenya arejeshwa nyumbani kwa udanganyifu



Kocha wa timu ya riadha ya Kenya inayoshiriki michuano ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro amerudishwa nyumbani kwa kosa la udanganyifu.
Mkuu wa Timu ya Olimpiki ya kenya, Kip Keino amesema John Anzrah aliigiza kama miongoni wa wakimbiaji wa mita 800, na kutoa sampuli ya mkojo kwa niaba ya mkimbiaji Ferguson Rotich.
Udanganyifu uligundulika na wakaguzi wa dawa za kusisimua misuli baada ya kuangalia picha za kitambulisho alichokuwa amevaa, ndipo walipogundua kuwa sura ya Bw Anzrah haeindani na mchezaji aliyefanya uchunguzi.
Mkuu wa Timu ya Olimpiki ya Kenya, Kipchoge Keino amesema uongozi wa timu yake hautavumilia tabia hiyo ingawa mpaka sasa hakuna hatua yoyote iliyotolewa dhidi ya Rotich.
Anzrah ni afisa wa pili kutoka kenya kurejeshwa nyumbani, wa kwanza akirudishwa kwa kosa la kuomba rushwa ili kuweza kukwepa upimaji wa matumizi ya dawa za kusisimua misuli.
Kumekuwa na idadi kadhaa ya wanariadha wa Kenya ambao walishindwa kufuzu vipimo vya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu huku ni wiki iliyopita tu shirika la kupambana na matumizi ya dawa hizo WADA likiiondoa Kenya kwenye nchi zilizoshindwa kutimiza masharti.  

TIMU YA AGLE NOIR KUFANYA ZIARA KANDA YA ZIWA





Timu ya Agle Noir (Black Eagles) ya Burundi leo Agosti 10, 2016 itaanza ziara ya kujiandaa na Ligi Kuu ya Burundi kwa kuweka kambi jijini Mwanza.
Timu hii maarufu kama Tai Weusi msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Burundi ilimaliza ikiwa ya nne kwenye msimu wa ligi nyuma ya Vital‘O na Inter Club.


Ikiwa nchini timu hii itacheza na timu iliyopinda daraja ya Mbao FC ambayo inanolewa na Kocha Mrundi Bwana, Etienne Ndairagije na pia watacheza na Toto African na timu ya kukuza vipaji ya Alliance ya Mwanza.


Baadaye watatembelea Shinyanga ambapo watapimana ubavu na kikosi cha Mwadui FC inayonolewa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

MABADILIKO KIDOGO LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA




Kutokana na sababu mbalimbali, Bodi ya Ligi (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imelazimika kubadili Ratiba ya Ligi Kuu kwa michezo kadhaa ya mwanzo kama ifuatavyo.
1. Mchezo Na. 2 - Kagera Sugar vs Mbeya City (20.08.2016)

Mchezo huo sasa utachezwa tarehe 21.08.2016 katika Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga. Sababu ni kuwa uwanja wa Kaitaba bado utakuwa kwenye matengenezo.
 2. Mchezo Na.4 - Toto African vs Mwadui FC (20.08.2016)

Mchezo huo sasa utachezwa tarehe 24.08.2016 katika Uwanja wa CCM Kirumba. Sababu za mabadiliko ni kuwa uwanja huo tarehe 20.08.2016 utakuwa na matumizi mengine ya kijamii.
3. Mchezo Na.13 - Kagera Sugar vs Stand United (27.08.2016)

Mchezo huo sasa utachezwa katika Uwanja wa CCM Kambarage. Awali timu mwenyeji wa mchezo huo ilikuwa ni Kagera Sugar, lakini kwa sasa timu mwenyeji atakuwa ni Stand United.
4. Mchezo Na.55 - Toto vs Ndanda (02.10.2016)

Mchezo huo sasa utachezwa tarehe 03.10.2016 badala ya tarehe 02.10.2016
5. Mchezo Na.80 - Mbao FC vs Ndanda fc (16.10.2016)

Mchezo huo umerudishwa nyuma kutoka tarehe 16.10.2016 hadi tarehe 28.09.2016. Sababu ni kuiwezesha timu ya Ndanda kucheza michezo miwili kwa kanda ya ziwa kwa lengo la kupunguza gharama.
6. Mchezo Na.96 - Tanzania Prisons vs Mbao FC (22.10.2016)



Mchezo huo sasa utachezwa tarehe 23.10.2016 badala ya 22.10.2016 ili kuipa nafasi timu ya Mbao kupumzika na kusafiri. Tayari timu za Ligi Kuu ya Vodacom zimearifiwa na kuagizwa kuzingatia mabadiliko hayo.
Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com