Monday, August 29, 2016

Kocha Azam FC aridhishwa na vipaji Temeke, sasa zamu ya U-17 Ilala Jumamosi ijayo


MKUU wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, ameridhishwa na viwango vya wachezaji vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17) kutoka Wilaya ya Temeke na Kigamboni waliojitokeza kwenye majaribio yaliyofanyika jana Jumapili ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Azam FC imeanza mchakato rasmi wa kuunda kizazi kipya cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, mpango ambao itazunguka mikoa 13 nchi nzima, ambapo kwa kuanzia tayari imefanikiwa kumaliza majaribio ndani ya eneo la Wilaya ya Temeke na Kigamboni, wakijitokeza vijana 423 na kuchaguliwa watano tu.
Legg ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc kuwa mara baada ya zoezi hilo kukamilika kwa mafanikio makubwa kwenye maeneo hayo mawili, hivi sasa amewakaribisha vijana wa umri huo kutoka Wilaya ya Ilala watakaotakiwa kujitokeza kwa wingi ndani ya Uwanja wa Jakaya Kikwete Park (JMK Park) Jumamosi ijayo Septemba 3 mwaka huu.
Vijana hao watatakiwa kufika kwa ajili ya majaribio hayo kuanzia saa 1.00 asubuhi wakiwa na vyeti vyao vya kuzaliwa na wazazi au walezi wao, ambao watawaongoza na kuwashuhudia wanapoonyesha viwango vyao pamoja na kutoa msaada wowote wa kumwelezea kijana wake pale itakapohitajika.
“Kulikuwa na viwango vizuri leo (jana), tulitarajia kupokea vijana zaidi takribani 500 hapa lakini wamejitokeza 423, lakini tunaamini tutapata vijana zaidi kwa majaribio ya pili Wilaya ya Ilala ndani ya JMK Jumamosi ijayo.
“Viwango vilikuwa vizuri, hususani dakika 45 za mwisho kwenye mechi iliyohusisha vijana 23 tuliowachagua hadi mchujo wa mwisho na hatimaye kupata watano wa mwisho, hatukuweza kuchagua wengi zaidi kwa kuwa tunachagua vijana bora zaidi Tanzania nzima, lakini tumeshuhudia viwango vizuri sana,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com