Saturday, November 19, 2016

LANGA LESSE BERCY WA KONGO - BRAZZAVILLE AINGIA MITINI VIPIMO VYA UMRI CAF


MCHEZAJI wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Kongo- Brazzaville, Langa Lesse Bercy ameshindwa kuwasili Cairo, Misri kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na uchunguzi juu ya umri wake kama alivyotakiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimkatia Rufaa CAF Langa Lesse Bercy baada ya kujiridhisha amevuka umri wa kucheza mashindano ya U-17.
Na hiyo ilifuatia Kongo- Brazzaville kuitoa Tanzania, Serengeti Boys katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania fainali za U-17 Afrika mwakani nchini Madagascar. 


Kutokana na rufaa hiyo, Langa Lesse Bercy alitakiwa na CAF kufika makao makuu ya shirikisho hilo, Cairo, Misri kwa ajili ya kurudia na kuthibitisha umri wake kwa kipimo cha MRI (Magnetic Imaging Resonance).
Na TFF ilikubali sharti la CAF kugharamia zoezi zima ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za usafiri wa mchezaji husika na daktari wake  pamoja na kulipia gharama za vipimo.


Wakati zoezi la vipimo limepangwa kufanyika leo, Shirikisho la Soka la Kongo- Brazzaville limetoa taarifa kwamba Langa Lesse Bercy hataweza kutokea kwa sababu ambazo ziko nje ya uwezo wao.
Zoezi limepangwa kufanyika leo kuanzia Saa 5.00 asubuhi mjini Cairo, Misri. Ujumbe wa TFF wa watu wanne ukiambatana na madaktari wawili uliwasili mjini Cairo tangu Novemba 17, 2016 ili kuwa shuhuda wa zoezi la kipimo hicho.
Na jana usiku saa 5.00 TFF ilipokea ujumbe kutoka CAF kuwa mchezaji Langa Bercy ameshindwa kusafiri kwenda Cairo kwa kuwa yuko katika eneo lililoko "vitani",eneo hilo halikutajwa.
Taarifa ya TFF kwa vyombo vya Habari leo, imesema kwamba wanaendelea kufuatilia kwa karibu jambo hili ili kuhakikisha haki inatendeka .

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com