Monday, September 5, 2016

AZAM FC YATUA SALAMA JIJINI MBEYA KUKABILIANA NA MBEYA CITY



 BAADA ya safari ndefu ya takribani saa 16, hatimaye kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kimewasili salama jijini Mbeya saa 2 usiku huu kikiwa na morali kubwa ya kuibuka ushindi kwenye mechi zake mbili mkoani hapa.
Azam FC imetua mkoani humu kwa malengo ya kubeba pointi sita kwenye mechi zake za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Tanzania Prisons (Septemba 7) na Mbeya City (Septemba 10), zitakazofanyika Uwanja wa Sokoine.
Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez na wasaidizi wake Yeray Romero (Kocha Msaidizi), Pablo Borges (Kocha Msaidizi wa Viungo), Jose Garcia (Kocha wa Makipa), Sergio Perez (Mtaalamu wa Tiba za Viungo) na Martine Valentine (Daktari), wameondoka na nyota wote wa kikosi hicho.
Nyota hao waliowasili hapa ni Kipa Mwadini Ally, mabeki Aggrey Morris, Pascal Wawa, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Ismail Gambo, Gadiel Michael, viungo Frank Domayo, Michael Bolou, Mudathir Yahya, Abdallah Masoud, Ramadhan Singano, Khamis Mcha pamoja na washambuliaji Francisco Zekumbawira na Gonazo Bi Thomas.
Wachezaji wengine waliokuwa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Aishi Manula, David Mwantika, Himid Mao, John Bocco na Jean Mugiraneza aliyeko Rwanda 'Amavubi, hao wanatarajia kutua mkoani hapa kesho Jumatatu asubuhi kwa usafiri wa ndege.
Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji chenye ladha safi inayochangamsha mwili Azam Cola, kikiwa mkoani hapa kimeweka kambi yake katika Hoteli ya Manyanya yenye utulivu mkubwa.

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com