Leo Agosti 5, 2016, michezo ya 31 ya Olimpiki itafunguliwa rasmi jijini Rio nchini Brazil. Tanzania itakuwepo!
Katika michezo ya mwaka huu, Tanzania itawakilishwa na wanamichezo
saba; wanariadha wanne, waogeleaji wawili na mwanajudo mmoja. Timu ya
Tanzania inakwenda Rio kinyonge tena kwa mafungu mafungu huku nyuso za
mashujaa wetu zikihadithia simulizi tofauti na ndimi zao. Ndimi
zimeahidi medali lakini nyuso zimekataa. Tanzania inasikitisha!
Hii ni tofauti na ilivyokuwa miaka 40 iliyopita, 1976, siku moja
kabla ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki. Tanzania ilikuwa Tanzania
kweli kweli. Tanzania ilikuwa moto!
Siku hiyo ilikuwa Julai 16, 1976, siku moja kabla ya kufunguliwa
rasmi kwa michezo ya 21 ya Olimpiki huko Montreal Canada, (kama
ilivyokuwa jana, siku moja kabla ya ufunguzi wa Olimpiki ya Rio) dunia
ilipata mtikisiko kwa kauli moja tu kutoka Tanzania, “HATUTASHIRIKI
OLIMPIKI MWAKA HUU”. Tanzania ilikuwa thabiti.
Kauli hiyo iliyotolewa na Ikulu ya Magogoni, ilipeleka mwangwi dunia
nzima na kuzua mtikisiko mkubwa uliopelekea mataifa 28 ya Afrika na
mengine matano kutoka nje ya Afrika, kuitikia wito wa Tanzania wa
kususia michuano hiyo. Kati ya mataifa hayo, 20 yalikuwa tayari
yameshawasili Montreal lakini yakaitikia wito wa Tanzania na kurudi
majumbani kwao. Tanzania ilisikilizwa. Tanzania iliheshimika!
Tido Mhando, mtangazaji wa kipindi cha michezo RTD wakati huo, ambaye
alikuwa asafiri na timu ya Tanzania, anakumbuka vizuri tukio hilo.
“Tulikuwa tumejiandaa vizuri. Tanzania ilikuwa na timu ya wachezaji
zaidi ya 40 akiwemo Filbert Bayi ambaye alikuwa nyota mkubwa kabisa
duniani. Wakati huo, ukiwataja wanamichezo maarufu duniani,
utamzungumzia Muhammad Ali kwenye masumbwi, Yohan Cruyff kwenye mpira na
Filbert Bayi kwenye riadha. Na kwa kuwa hao wengine hawakushiriki
Olimpiki, Filbert Bayi ndiyo alikuwa nyota mkubwa zaidi kwenye Olimpiki
hizo”. Tanzania iliheshimika. Tanzania iliogopewa!
Kwa maelezo ya Tido, Bayi alitoka kushinda medali ya dhahabu ya
michezo ya Jumuiya ya Madola huko Christchurch New Zealand 1974 ambako
aliweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 akitumia muda wa dakika 3
na sekunde 32.16, rekodi ambayo imedumu mpaka sasa. Kikubwa hapa
hakikuwa tu rekodi bali mtindo alioutumia kuiweka…Bayi alikimbia kwa
kasi ileile tangu anaanza mpaka anamaliza akimuacha mpinzani wake wa
karibu, John Walker, aliyekuwa uwanja wa nyumbani. Tanzania ilitikisa!
“Nikiwa kama mtangazaji wa michezo, nilipewa taarifa kwamba kuna
kikao kikubwa cha serikali kikiongozwa na Rais, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, kujadili hatima ya Tanzania kwenye olimpiki hizo. Hayupo
aliyejua kwamba kikao hicho kitatoka na kauli gani hivyo mimi binafsi
kama mwanahabari na wanamichezo washiriki tuliambiwa tuwe tayari tayari
kwa lolote. Baadaye zikaja taarifa kwamba serikali imeamua kutoshiriki.
Taarifa hizo nikazi-break mimi kupitia kipindi changu cha michezo na
hapo hapo zikasambaa duniani. BBC na mashirika mengine makubwa duniani
yakaninukuu….kilichofuata baada ya hapo ni hasara kubwa kwa jiji
mwenyeji la Montreal. Wanamichezo zaidi ya 300 walijiondoa na
kusababisha michezo mingi kufutwa”. Anakumbuka Tido Mhando ambaye sasa
ni afisa mtendaji mkuu wa Azam Media.
Kisa cha Tanzania kususia michezo hiyo ni kupinga kitendo cha kamati
ya kimataifa ya Olimpiki, IOC, kuiruhusu New Zealand kushiriki Olimpiki
hizo ilhali ilikiuka maagizo yake ya kuitenga Afrika Kusini kutokana na
sera zake za ubaguzi wa rangi.
Afrika Kusini ilitengwa na IOC tangu 1964, lakini timu ya taifa ya
ragga ya New Zealand (All Blacks) ilifanya ziara ya kirafiki nchini
humo. Kitendo hicho kilitafsiriwa kama kupuuza maagizo ya dunia ya
kuitenga Afrika Kusini.
Tanzania kama kinara wa kupinga ubaguzi, ilikuwa ikisubiriwa itakuja
na tamko gani…hatimaye tamko likatoka na kuitikiwa barabara.
Tanzania iliyokuwa na nyota mkubwa kabisa, Filbert Bayi, ilikuwa
ikitazamwa kama moja ya mataifa yatakayong’arisha Olimpiki hiyo.
Jaribu kuifikirikia Tanzania ya sasa yenye timu ya wanamichezo saba
tu. Wanamichezo wenye majina madogo, siyo tu kimataifa bali hata
kitaifa. Siyo ajabu katika watu kumi, ni mtu mmoja pekee akawa anawajua
wawakilishi wetu.
Tanzania hii inaweza kweli kutoa kauli itakayoitikiwa na umma wa kimataifa?
Tanzania hii inaweza kweli kichukuliwa kama moja ya mataifa yatakayong’arisha michezo hiyo?