Saturday, August 6, 2016

Nafasi Ya Tanzania Ndani ya Olimpiki





Leo Agosti 5, 2016, michezo ya 31 ya Olimpiki itafunguliwa rasmi jijini Rio nchini Brazil. Tanzania itakuwepo!
Katika michezo ya mwaka huu, Tanzania itawakilishwa na wanamichezo saba; wanariadha wanne, waogeleaji wawili na mwanajudo mmoja. Timu ya Tanzania inakwenda Rio kinyonge tena kwa mafungu mafungu huku nyuso za mashujaa wetu zikihadithia simulizi tofauti na ndimi zao. Ndimi zimeahidi medali lakini nyuso zimekataa. Tanzania inasikitisha!
Hii ni tofauti na ilivyokuwa miaka 40 iliyopita, 1976, siku moja kabla ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki. Tanzania ilikuwa Tanzania kweli kweli. Tanzania ilikuwa moto!
Siku hiyo ilikuwa Julai 16, 1976, siku moja kabla ya kufunguliwa rasmi kwa michezo ya 21 ya Olimpiki huko Montreal Canada, (kama ilivyokuwa jana, siku moja kabla ya ufunguzi wa Olimpiki ya Rio) dunia ilipata mtikisiko kwa kauli moja tu kutoka Tanzania, “HATUTASHIRIKI OLIMPIKI MWAKA HUU”. Tanzania ilikuwa thabiti.
Kauli hiyo iliyotolewa na Ikulu ya Magogoni, ilipeleka mwangwi dunia nzima na kuzua mtikisiko mkubwa uliopelekea mataifa 28 ya Afrika na mengine matano kutoka nje ya Afrika, kuitikia wito wa Tanzania wa kususia michuano hiyo. Kati ya mataifa hayo, 20 yalikuwa tayari yameshawasili Montreal lakini yakaitikia wito wa Tanzania na kurudi majumbani kwao. Tanzania ilisikilizwa. Tanzania iliheshimika!
Tido Mhando, mtangazaji wa kipindi cha michezo RTD wakati huo, ambaye alikuwa asafiri na timu ya Tanzania, anakumbuka vizuri tukio hilo.
“Tulikuwa tumejiandaa vizuri. Tanzania ilikuwa na timu ya wachezaji zaidi ya 40 akiwemo Filbert Bayi ambaye alikuwa nyota mkubwa kabisa duniani. Wakati huo, ukiwataja wanamichezo maarufu duniani, utamzungumzia Muhammad Ali kwenye masumbwi, Yohan Cruyff kwenye mpira na Filbert Bayi kwenye riadha. Na kwa kuwa hao wengine hawakushiriki Olimpiki, Filbert Bayi ndiyo alikuwa nyota mkubwa zaidi kwenye Olimpiki hizo”. Tanzania iliheshimika. Tanzania iliogopewa!
Kwa maelezo ya Tido, Bayi alitoka kushinda medali ya dhahabu ya michezo ya Jumuiya ya Madola huko Christchurch New Zealand 1974 ambako aliweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 akitumia muda wa dakika 3 na sekunde 32.16, rekodi ambayo imedumu mpaka sasa. Kikubwa hapa hakikuwa tu rekodi bali mtindo alioutumia kuiweka…Bayi alikimbia kwa kasi ileile tangu anaanza mpaka anamaliza akimuacha mpinzani wake wa karibu, John Walker, aliyekuwa uwanja wa nyumbani. Tanzania ilitikisa!
“Nikiwa kama mtangazaji wa michezo, nilipewa taarifa kwamba kuna kikao kikubwa cha serikali kikiongozwa na Rais, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kujadili hatima ya Tanzania kwenye olimpiki hizo. Hayupo aliyejua kwamba kikao hicho kitatoka na kauli gani hivyo mimi binafsi kama mwanahabari na wanamichezo washiriki tuliambiwa tuwe tayari tayari kwa lolote. Baadaye zikaja taarifa kwamba serikali imeamua kutoshiriki. Taarifa hizo nikazi-break mimi kupitia kipindi changu cha michezo na hapo hapo zikasambaa duniani. BBC na mashirika mengine makubwa duniani yakaninukuu….kilichofuata baada ya hapo ni hasara kubwa kwa jiji mwenyeji la Montreal. Wanamichezo zaidi ya 300 walijiondoa na kusababisha michezo mingi kufutwa”. Anakumbuka Tido Mhando ambaye sasa ni afisa mtendaji mkuu wa Azam Media.
Kisa cha Tanzania kususia michezo hiyo ni kupinga kitendo cha kamati ya kimataifa ya Olimpiki, IOC, kuiruhusu New Zealand kushiriki Olimpiki hizo ilhali ilikiuka maagizo yake ya kuitenga Afrika Kusini kutokana na sera zake za ubaguzi wa rangi.
Afrika Kusini ilitengwa na IOC tangu 1964, lakini timu ya taifa ya ragga ya New Zealand (All Blacks) ilifanya ziara ya kirafiki nchini humo. Kitendo hicho kilitafsiriwa kama kupuuza maagizo ya dunia ya kuitenga Afrika Kusini.
Tanzania kama kinara wa kupinga ubaguzi, ilikuwa ikisubiriwa itakuja na tamko gani…hatimaye tamko likatoka na kuitikiwa barabara.
Tanzania iliyokuwa na nyota mkubwa kabisa, Filbert Bayi, ilikuwa ikitazamwa kama moja ya mataifa yatakayong’arisha Olimpiki hiyo.
Jaribu kuifikirikia Tanzania ya sasa yenye timu ya wanamichezo saba tu. Wanamichezo wenye majina madogo, siyo tu kimataifa bali hata kitaifa. Siyo ajabu katika watu kumi, ni mtu mmoja pekee akawa anawajua wawakilishi wetu.
Tanzania hii inaweza kweli kutoa kauli itakayoitikiwa na umma wa kimataifa?

Tanzania hii inaweza kweli kichukuliwa kama moja ya mataifa yatakayong’arisha michezo hiyo?

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com