Thursday, August 18, 2016

Mkuu wa Wilaya Kinondoni awapiga ‘STOP’ mgambo kuwafanyia fujo wafanyabiashara wadogo




Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi amewapiga marufuku mgambo wa wilaya hiyo kuwafanyia fujo wafanyabiashara wadogo wanaofanya shughuli zao katika maeneo rasmi.
Hapi aliyasema hayo jana katika kipindi cha Mada Moto kinachorushwa moja kwa moja na kituo cha Channel Ten.
Alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya watu kuwatoza ushuru kinyume cha sheria wafanyabiashara hao wanaofahamika kwa jina la wamachinga jambo linalosababisha halmashauri ya manispaa ya kinondoni kupoteza mapato.
“Kuna mtu mmoja alikuwa anatoza wamachinga ela, zaidi ya sh 8,000 kwa siku na walikuwa wanalipa, kama serikali ikiweka mfumo mzuri inaweza kupata mapato ya uhakika kutoka kwa wamachinga,” alisema.
Alisema atahakikisha anapata idadi ya wamachinga wote katika wilaya hiyo ili kuwawezesha kiuchumi ikiwemo kuwapa mikopo na kutenga siku ya gulio ili wapate fursa ya kufanya biashara.
“Machinga wote tuwatambue tuwaunganishe na bima ya afya, wapewe mikopo hakika watainuka sababu hakuna mtu aliyezaliwa kuwa machinga muda wote, tunataka Kuwainua ili waje kuwa wafanyabiashara baadae,” alisema.
“Ni marufuku kupiga na kuwasumbua wamachinga, kuwaibia bidhaa zao ni marufuku,” alisema.
“Sisi viongozi kazi yetu ni kuwaongoza na kuwaonyesha Mahala panapostahili wao kufanyakazi, na wilaya yangu ya kinondoni ina mkakati wa kuandaa magulio ili wafanyabiashara ndogondogo wauze bidhaa zao, ” alisema.
Aliongeza kuwa “Nyuma kulikuwa na mianya ya upotevu wa mapato, tumefanya kazi kubwa Na kamati ya usalama na sasa watu wanafurika kulipa kodi. “

“Tunawaomba watanzania watuombee kwa kuwa tunaopambana nao siyo wote wanafurahi. Wananchi washiriki katika kutoa taarifa za wakwepa kodi na kadhalika,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com