Mabalozi wafunguka kinachowakuna kwa JPM
Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, wamempongeza Rais Magufuli pamoja na serikali ya awamu ya tano kwa jitihada zake za kupambana na rushwa, kujenga nidhamu kwa watumishi wa umma na kuimarisha uchumi.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi
wenzake katika sherehe ya kuaga mwaka mpya kwa Mabalozi na Wawakilishi
wa mashirika ya kimataifa (New Year Diplomatic Sherry Party)
iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa wanadiplomasia hao
Mhe. Edzai Chimoyo ambaye ni Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, ameahidi
kuwa yeye na wenzake wapo tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Awamu
ya Tano.
Pia amepongeza juhudi kubwa zilizofanywa kufufua Shirika la Ndege (ATCL) kwa kununua ndege mpya ambazo licha ya kurahisisha usafiri zitasaidia kukuza sekta ya utalii hapa nchini.
Akihutubia sherehe hizo, Rais John
Magufuli amezialika nchi mbalimbali na wadau mbalimbali wa maendeleo
kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika
kujenga uchumi wa viwanda utakaoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi ya
kipato cha kati.
Mhe. Dkt. Magufuli amesema ifikapo mwaka
2020 Tanzania imedhamiria uchumi wake ukue kwa wastani wa asilimia 10,
sekta ya Viwanda iajiri asilimia 40 ya watanzania na pato la mtu kwa
mwaka likue hadi kufikia wastani wa Dola 3,000 za kimarekani (sawa na Shilingi na takribani shilingi Milioni 6 na Laki 6 kwa mwaka)
Pia amewaomba wawahamasishe wadau
watakaokuwa tayari kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi
ya ujenzi ikiwemo ujenzi wa reli ya kati yenye urefu wa Kilometa 1,200
kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge)kuanzia Dar es Salaam
hadi Mwanza na Kigoma na kuunganisha hadi nchi za Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda,na kwamba tayari Serikali itaanza
kujenga Kilometa 300 za kuanzia Dar es Salaam mwaka huu.
Kuhusu mwaka uliopita, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeanza kutekeleza awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo (2016-2021)
uliopangwa kugharimu Shilingi Trilioni 107 ambapo kati ya fedha hizo
Shilingi Trilioni 59 zitatolewa na Serikali ya Tanzania na kiasi
kinachobaki kitatolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mhe. Dkt. Magufuli amebainisha kuwa
katika kutekeleza mpango huo, Serikali imechukua hatua ya kuongeza
bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 26 hadi kufikia asilimia 40 katika
mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment