Huyu Ndege aliyesafiri kutoka Finland hadi Uganda
Ndege mmoja ambaye inaaminika alitoka nchini Finland amepatikana katika uwanja wa ndege wa Entebbe nchini Uganda.
Ndege
huyo aina ya Osprey kwa sasa anatunzwa na maafisa wa kituo cha
kuwahudumia wanyama cha Uganda Wildlife Education Centre (UWEC).Ndege huyo mkubwa, aina ya mwewe, aligunduliwa na maafisa wa uwanja wa ndege katika njia inayotumiwa na ndege kupaa na kutua katika uwanja wa huo wa Entebbe.
Isaac Mujaasi, afisa wa mauzo na mawasiliano katika UWEC, ameambia BBC kwamba ndege huyo alikuwa ameumia katika mabawa yake baada ya kugongwa na ndege iliyokuwa inapaa.
Alikuwa na pete yenye maelezo kumhusu mguuni ambayo inaashiria kwamba alimilikiwa na makumbusho ya historia asilia nchini Finland.
Bw Mujaasi anasema waliwasiliana na maafisa wa makumbusho hao ambao wamethibitisha kwamba ndege huyo ni wao.
“Hili lilituthibitishia kwamba ndege huyu alisafiri kutoka Helsinki, Finland,” Bw Mujaasi amesema. “Tutamtibu ndege huyo na akipona tutamwachilia na huenda akarejea kwao.”
Afisa huyo hata hivyo amesema ni kawaida kwa ndege kuhama kutoka Ulaya, hasa wakati wa majira ya baridi na kukimbilia maeneo yenye joto.
0 comments:
Post a Comment