Wednesday, May 10, 2017

HIMID MAO APEWA DAKIKA 90 DENMARK TIMU YAKE YAPIGWA 2-0


 Himid Mao Mkami leo amejumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji wa akiba na timu ya Randers FC ya Denmark na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Horsens.

Kiungo huyo wa Azam FC ya Dar es Salaam ambaye yupo Denmark kwa majaribio ya kujiunga na timu hiyo ya Ligi Kuu, amecheza kwa dakika zote 90 na kwa bahati mbaya wachezaji wa akiba wa Randers FC wakafungwa 2-0.


" Himid amesema kwamba ulikuwa mchezo mgumu, lakini upande wake anamshukuru Mungu amecheza vizuri."

“Unajua kufungwa haimaanishi mmecheza vibaya, wakati mwingine mnaweza kucheza vizuri kuliko waliowafunga, sema basi tu mambo ya mpira,”amesema Himid, mtoto wa kiungo wa zamani wa Pamba, Mao Mkami ‘Ball Dancer’.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Tanzania amesema baada ya kufanya mazoezi na timu hiyo kwa takriban siku tatu na leo kucheza mechi ya kwanza – kesho anatarajiwa kupewa ratiba mpya.


Himid amesema anaamini baada ya kucheza Tanzania kwa muda mrefu, sasa ni wakati mwafaka kwake kutoka nje.
“Ni kweli nina nia sana ya kutoka nje kwa sasa, naamini ni wakati mwafaka kwangu kupata changamoto mpya katika maisha yangu ya soka,”amesema Nahodha huyo Msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.   

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com