Thursday, November 17, 2016

SIKILIZA ASICHOSEMA MGHANA WA AZAM BAADA USAJILI


NYOTA mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yahaya Mohammed, amesema kuwa amejiunga na timu hiyo kwa kazi moja tu kuipigania timu ili kupata matokeo bora uwanjani.
Mohammed jana jioni alikamilisha usajili wa kujiunga na timu hiyo akisaini mkataba wa miaka miwili tayari kabisa kuitumikia Azam FC kuanzia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Kombe la Kagame ikiwa kama bingwa mtetezi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, 28, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mashabiki wa Azam FC wake mkao wa kufurahi kwani kwa kushirikiana na wachezaji wenzake watafanikiwa kuwapa furaha kwa kupata matokeo bora uwanjani.
“Ninafuraha kubwa kusaini mkataba wa kujiunga na Azam FC, nimejipanga kukabiliana na changamoto zote hapa kwani ukiwa mchezaji ni kazi yako na unapaswa kujiandaa na hilo na kila muda unapaswa kujiandaa na kazi yako,” alisema.
Staa huyo pia alichukua fursa hiyo kuomba sapoti kwa mashabiki wa timu hiyo, waendelee kuisapoti Azam FC kwani hilo litawapa nguvu wao kama wachezaji kuweza kufanya vizuri uwanjani na kupambana kwa ajili ya matokeo bora.
“Tunahitaji sapoti yao na waendelee kuipa sapoti Azam FC, hilo litatufanya sisi kuipeleka timu mbele zaidi, sisi pekee wachezaji hatuwezi kuipeleka timu mbele kama mashabiki hawatusapoti, tunawahitaji sana na sisi wanatuhitaji, waisapoti timu katika hali mbaya na nzuri kwani hii ni timu yao, sisi tutaingia uwanjani kucheza kwa ajili yao na tunawaahidi tutawapa furaha kwa matokeo mazuri,” alisema.
Akizungumzia kuhusu soka la Tanzania, aliongeza kuwa: “Kwa sasa sijui lolote kuhusu soka la Tanzania kwani nikiwa Ghana hakuna kituo cha televisheni kinachoonesha ligi ya hapa, ila kwa sasa mimi ni mwanafamilia wa Azam FC, hilo sio tatizo kwangu ukiwa kama mchezaji unatakiwa kusimama popote na kucheza na kufanya vizuri kwa ajili ya klabu.”
Straika huyo anatarajia kuanza rasmi mazoezi Desemba 3 mwaka huu, wakati kikosi hicho kitakaporejea kutoka likizo ya wiki mbili, ambapo kesho Ijumaa atarejea nchini kwao Ghana kwa ajili ya kujipanga zaidi pamoja na mapumziko mafupi.
Mbali na kuiongoza Aduana Stars kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita, Mohammed pia aliiibuka mfungaji bora namba mbili wa ligi hiyo kwa mabao 15 aliyofunga nyuma ya Latif Blessing wa Liberty Proffesional aliyetupia 17.
Mohammed alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika mwaka juzi nchini Afrika Kusini na timu hiyo kuwa washindi wa pili akiwa pamoja na straika mwingine aliyesajiliwa na Azam FC, Samuel Afful.

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com