TAIFA STARS KUJIPIMA NA ETHIOPIA
Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars), inatarajiwa kucheza na Ethiopia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Oktoba 8, 2016.
Mchezo huo utakaofanyika jijini Addis Ababa, umeratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo huwa na kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa kwa wanachama wake – Tanzania ni miongoni mwao. Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ethiopia (EFF), wameomba mchezo huo ufanyike kwao.
Hii ni faida kwa Tanzania kama itashinda mchezo huo kwa maana kina alama za nyongeza kama inatokea unaifunga timu mwenyeji.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa atakuwa na nafasi ya kuandaa kikosi chake kuanzia Oktoba 3, 2016 mara baada ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambako Mwadui itacheza na Azam huku Mbao ikishindina na JKT Ruvu Oktoba 2, mwaka huu kabla ya kupisha kalenda hiyo ya FIFA ya michuano ya kimataifa.
Matokeo ya mchezo huo, ni sehemu malumu kupima viwango vya ubora na uwezo wa timu za taifa. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 132 kati ya nchi 205 wanachama wa FIFA zilizopimwa ubora. Ethiopia yenyewe inashika nafasi ya 126.
Argentina inaongoza ikifuatiwa na Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta – nyota wa kimataifa wa Tanzania. Samatta anacheza klabu ya K.R.C Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji. Timu nyingine bora kimataifa ni Ujerumani, Colombia na Brazil.
Katika Bara la Afrika, Ivory Coast ambayo ni ya 34 kwa ubora duniani ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Algeria, Senegal, Tunisia na Ghana.
0 comments:
Post a Comment