Friday, August 12, 2016

Wafahamu vijana 10 wa chini ya miaka 30 walio matajiri zaidi duniani




Tajiri mmiliki wa ardhi ambaye pia amekuwa akisaidia wasiojiweza katika jamii, Mtawala wa Westminister Gerald Cavendish Grosvenor amefariki na kumwachia mwanawe Hugh Grosvenor urithi wa £9bn.
Alikuwa na binti watatu, na mwana mmoja pekee wa kiume, Hugh, mwenye umri wa miaka 25.
Hugh amerithi "nusu ya London" kwani ardhi nyingi maeneo mengi ya Belgravia na Mayfair, London ilimilikiwa na babake.
Yeye hufanya kazi katika kampuni ya Bio-bean, kampuni inayoangazia teknolojia isiyoongeza gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani.
Kwa mujibu wa orodha ya jarida la Forbes ya mwaka 2016, kuna vijana wengine tisa wa chini ya umri wa miaka 30 ambao utajiri wao ni zaidi ya dola bilioni moja za Marekani.
Vijana wengine matajiri ni:
2 & 3: Alexandra, 20, na Katharina Andresen, 21
Ndio wachanga zaidi na wanamiliki kampuni ya Ferd.
Binti hawa walirithi utajiri hu kutoka kwa baba yao Johan, raia wa Norway mwaka 2007.
4: Gustav Magnar Witzoe, 23
Anatoka Norway pia na huonesha maisha yake ya kifahari kwenye Instagram.
Amerithi sehemu ya biashara ya babake ya kufuga samaki na sasa utajiri wake ni $1.1bn (£846m).
Gustav Witzoe, babake ambaye wana jina sawa, alimpa hisa kwenye kampuni hiyo kama zawadi. Lakini hana udhibiti au usemi wowote.
5&6: Ludwig Theodor Braun na dadake
Haonekani sana mtandaoni. Hayupo kwenye Twitter au Instagram lakini anatambuliwa kwa utajiri.
Familia yake ilianzisha kampuni ya dawa ya B. Braun Melsungen, Ujerumani 1839.
Kampuni hiyo ni maarufu sana kwa dawa na vifaa vya matibabu.
Ludwig humiliki 10% ya kampuni hiyo ambayo ni sawa na $1.8bn (£1.4bn).
Dadake Eva Maria Braun-Luedicke yuko nyuma yake kidogo lakini utajiri wake ni $1.4bn (£1bn).

7&8: Waanzilishi wa Snapchat


Image copyright Getty Images
Image caption Waanzilishi wa Snapchat Evan Spiegel na Bobby Murphy
Evan Spiegel ni mmoja wa walioanzisha mtandao wa Snapchat ambao hutumiwa na mamilioni ya vijana duniani.
Majuzi, aliingia uchumba na mwanamitindo mashuhuri duniani Miranda Kerr.

Image copyright Getty Images
Ana umri wa miaka 26 na utajiri wake ni $2.1bn (£1.6bn), Evan ndiye mchanga zaidi miongoni mwa waanzilishi wa Snapchat na ndiye tajiri zaidi miongoni mwao.
Mwenzake ni Bobby Murphy, 28, ambaye anamkaribia sana kwa utajiri.
Utajiri wa Murphy ni $1.8bn (£1.3bn).
9: Lukas Walton
Kwa mujibu wa Forbes, Lukas Walton, 29, ndiye anayemkaribia sana Hugh Grosvenor.
Utajiri wake ni $10.4bn, ambazo ni karibu £7.2bn kwa viwango vya sasa vya ubadilishanaji wa fedha vya sasa.
Anatoka katika familia tajiri inayomiliki Walmart (miongoni mwa kampuni nyingine), ambayo pia humiliki Asda nchini Uingereza.
10: Wang Han
Wang Han, raia wa China, anakamilisha orodha hii.
Chanzo cha utajiri wake ni urithi wa hisa za kampuni ya ndege ya Juneyao Air kutoka kwa babake Wang Junyao, aliyefariki 2004.
Junyao alikuwa mwanzilishi wa kampuni ya Juneyao Group. Wang Han humiliki 27% ya hisa za shirika hilo la ndege na 14% ya hisa za maduka ya jumla ya Wuxi Commercial Mansion Grand Orient.
Utajiri wake unakadiriwa na Forbes kuwa $1.34bn.

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com