Friday, August 12, 2016

Gazeti la Mseto nje kwa miaka 3




Serikali nchini Tanzania imelifungia gazeti la kila wiki la Mseto kuchapishwa katika njia zote ikiwa ni pamoja na mitandao. Hili ni gazeti la pili kufungiwa ndani ya mwaka mmoja.
Serikali inasema Mseto limekuwa likiandika taarifa za uongo na kugushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za serikali huku taarifa hizo zikiwa na nia ya uchochezi na kumchafua Rais John Magufuli na viongozi wengine wa serikali yake.
Akitangaza kufungiwa kwa gazeti hili mapema leo hii, Waziri mwenye dhamana ya habari Nape Nnauye amewaambia waandishi wa habari kuwa amelifungia gazeti hilo kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976
Hakuna taarifa rasmi yoyote ya mwitikio wa kufungiwa huko kutoka kwa wachapishaji na wamiliki wa gazeti hilo
Hili ni gazeti la pili kufungiwa ndani ya mwaka mmoja. Mwezi Januari mwaka huu, serikali ililifungia pia gazeti la Mawio muda wote.
Wasiwasi miongoni mwa wadau wa habari umeendelea kuongezeka kwa kile kinachoonekana kuwa utawala huu mpya unaviminya vyombo vya habari na kukandamiza uhuru wa kutoa na kupokea habari pia hapa nchini Tanzania.
Tayari watu wawili wameshtakiwa baada ya kuandika jumbe katika mitandao ya kijamii zilizoonekana kumtusi Rais Magufuli
Inawezekana kufungwa huku kwa gazeti la Mseto kutaibua ukosoaji hasa kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu ambao wamekuwa wakiikosoa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo wanasema inatoa mamlaka makubwa sana kwa serikali kuminya uhuru wa habari nchini 

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com