Mataifa 10 yenye watu warefu zaidi duniani yaorodheshwa
Utafiti mpya umeonesha kwamba wanaume wa Uholanzi ndio warefu zaidi duniani, na upande wa wanawake, wanawake wa Latvia ndio warefu zaidi.
Utafiti huo, ambao matokeo yake yamechapishwa kwenye jarida la eLife, umefuatilia kimo cha watu na mabadiliko yaliyotokea katika mataifa 187 tangu 1914.
Utafiti huo umebaini kwamba wanaume wa Iran na wanawake wa Korea Kusini ndio walioongeza kimo zaidi, wakiongeza kimo cha wastani kwa zaidi ya inchi 6 (sentimeta 16) na inchi 8 (sentimeta 20) mtawalia.
Wanawake wafupi zaidi duniani wanapatikana nchini Guatemala huku wanaume wafupi wakitokea Timor Mashariki.
Mwanamke wa umri wa miaka 18 kwa wastani nchini Guatemala alikuwa na kimo cha futi 4 inchi 7 (sentimita 140) mwaka 1914 utafiti wa kwanza ulipofanywa na sasa kiwango hicho hakijafika kabisa futi 4 inchi 11 (sentimita 150).
Kimo cha wastani kwa wanaume Timor Mashariki ni futi 5 inchi 3 (sentimita 160).
Watafiti hao wanasema kuwa chembe chembe za jeni hubadilikabadilika, lakini cha muhimu zaidi ni kuwepo kwa lishe bora, usafi na matibabu ya hali ya juu.
Mataifa yenye wanaume warefu zaidi duniani 2014 (kwenye mabano ni nafasi iliyoshikiliwa 1914):
- Uholanzi (12)
- Ubelgiji (33)
- Estonia (4)
- Latvia (13)
- Denmark (9)
- Bosnia na Herzegovina (19)
- Croatia (22)
- Serbia (30)
- Iceland (6)
- Jamhuri ya Czech (24)
Mataifa yenye wanawake warefu zaidi duniani 2014 (kwenye mabano ni nafasi iliyoshikiliwa 1914):
- Latvia (28)
- Uholanzi (38)
- Estonia (16)
- Jamhuri ya Czech (69)
- Serbia (93)
- Slovakia (26)
- Denmark (11)
- Lithuania (41)
- Belarus (42)
- Ukraine (43)
0 comments:
Post a Comment