STANDARD BANK SMELL CORRUPTION IN AFRICA
Ufisadi kwa kiasi kikubwa unahusishwa na watu wenye madaraka ya kisiasa, taaluma, wenye uwezo wa kifedha na kiuchumi ambao hutumia uwezo huo kujineemesha na kujipatia mafao na masilahi wasiyostahili, hasa kwa njia za kihalifu na kuvunja sheria za nchi na kimataifa.
Hata
hivyo, taasisi na mashirika makubwa ya uchumi ya Kimataifa yanatumiwa
na wajanja kuendeleza vitendo vya uhalifu na kifisadi. Pale mashirika na
taasisi yanapobanwa na ufisadi wao kutambuliwa, hutafuta njia za
kutokea. Kama kawaida hutatafutwa mbuzi wa sadaka (bangusilo) ili
kutuliza mizimu.
Taaasisi ya Kimataifa ya Uchunguzi na
Uraghibishaji dhidi ya Vitendo va Rushwa (Corruption Watch) imefanya
uchambuzi wa kina na kutoa angalizo, mapitio na maoni kuhusu kuhusika
kwa benki ya kimataifa ya Standard iliyoko London katika ufisadi ambao
benki hiyo imekiri na kujishtaki kwa vyombo vya uchunguzi wa makosa
makubwa ya jinai (SFO).
Uamuzi huo umefanywa kwa msingi
wa sheria za Uingereza (Deferred Prosecution Agreement). Kwa mujibu wa
sheria hiyo, taasisi au shirika la biashara linapogundua kwamba ndani
yake kuna makosa ya jinai yaliyotendeka, huchukua hatua za kutafuta
makubaliano na upande wa mashtaka ili tuhuma ziainishwe na mahakama itoe
adhabu kwa kuzingatia kwamba mhusika anachotaka kufanya ni kurekebisha
tabia yake na arudi katika njia iliyochaguliwa ya kutii sheria.
Mambo
mengi yameandikwa na watu wameshangaa kwa Tanzania kujikuta katika
kashfa na ufisadi mwingine wa mabilioni ya fedha kuchotwa kwa ushiriki
wa Benki ya Standard kwa kupitia benki yake ya hapa nchini. Mpango
wenyewe ulikuwa kwamba Standard inunue dhamana ili upatikane mkopo wa
Dola 600 milioni za Marekani (sawa na Sh1.4 trillioni) kwa Serikali ya
Tanzania kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Kesi hii,
ambayo ina mchakato mrefu tangu mwaka 2011, imehusisha mawaziri wawili:
Mustafa Mkullo na marehemu Dk William Mgimwa kwa nyakati tofauti.
Kilicho wazi ni kwamba Tanzania inahitaji utaalamu wa kujifunga katika
mikataba mikubwa ya kimataifa; iwe ya madini, uchimbaji gesi na ununuzi,
benki na kampuni za kimataifa zinatambua udhaifu huo na licha ya
kuutambua, kila mara yako kwenye maabara ya kubuni bidhaa mpya kwa
madhumuni ya kujiongezea faida katika biashara zao, bila kujali gharama
watakayopata washirika na wateja wao.
Katika hili la
Benki ya Standard, kuna mambo muhimu ambayo ni muhimu wasomaji wayajue.
Yale ambayo Benki ya Standard imeyafanya kuyaandika na kuyasambaza ni
upande mmoja wa shilingi. Lakini kwa kuyazingatia na kujua matukio na
kuyapa matukio hayo tafsiri kama ilivyofanya Corruption Watch ndiyo njia
sahihi ya kuwahabarisha Watanzania na Serikali ya Awamu ya Tano kwamba
nyuma ya pazia la sakata la Benki ya Standard kuna mengi yamefunikwa.
Tunayaandika na kuyaelezea ili yajulikane, haki itendeke na Tanzania isiendelee kuwa uchochoro wa mtaji wa kimataifa.
Mambo
ya kuzingatia katika mfululizo wa makala haya ni kama ifuatavyo: Benki
ya Kimataifa ya Standard ambayo inamiliki na kudhibiti benki za Standard
na Stanbic Tanzania ni mojawapo ya taasisi kubwa za kibenki duniani
yenye kufanya shughuli zake kubwa kwenye Jiji la London.
Shughuli
zake nyingine kubwa ziko pia New York, Frankfurt, Hong Kong na
Johannesburg nchini Afrika Kusini. Ina leseni ya kufanya biashara ya
kimataifa ya kibenki jijini London na kwingineko. Kimuundo na kiutawala,
habari, shughuli na ruksa kwa kila kitu kinachofanyika kinapelekwa
London kwa uamuzi na maelekezo.
Hakuna kinachoweza
kufanyika bila ya ruksa kutoka London. Hivyo lilipotokea hili la tuhuma
na madai kuhusiana na kutoa rushwa ili Benki ya Standard ipewe zabuni na
Serikali ya Tanzania, benki hiyo ilijua wapi pa kukimbilia ili
kujikosha.
Benki hiyo ilikimbilia kwenye vyombo vya
sheria vya Uingereza (Serious Fraud Office) SFO na “kujishtaki” kwa
msingi wa sheria ijulikanayo kama Deferred Prosecution. Sheria hii
inatoa nafasi kwa mhusika kukiri mbele ya vyombo vya uchunguzi wa makosa
ya jinai na kutoa maelezo yote ya hujuma bila kushurutishwa na mwishowe
kukubali kushitakiwa, kwa mategemeo kwamba mhusika atapewa adhabu isiyo
kubwa ili aweze kurekebisha tabia na kurudi kwenye mstari.
Swali
la kujiuliza ni kwa nini Standard iliamua kujishtaki au “kujilipua” kwa
Kiswahili cha kileo? Bila kuingia kwa undani, ni wazi benki hiyo ilijua
fika kwamba kama ingelishtakiwa kwa njia za kawaida, kosa la kutoa
rushwa ili kupata zabuni ni kubwa kwa sheria za Uingereza na hivyo
adhabu yake ni kubwa.
Hapa tunafikiria adhabu ambayo
inaweza kutolewa kuwa ni pamoja na kufungiwa leseni ya kufanya biashara
ya kifedha katika Jiji la London. Adhabu nyingine ambazo zinaweza
kutolewa ni pamoja na kutozwa faini kubwa kama inavyofanyika Marekani.
Vilevile kuamriwa kurejesha mkopo wa Dola 600 milioni na gharama
nyingine kwa wale wafanyabiashara binafsi walionunua dhamana.
Kubwa
ya yote ni pamoja na uwezekano wa kukwama kwa mpango wa uliokuwa
umeshatayarishwa wa kuiuza Benki ya Standard kwa Wachina kwa sababu
benki ingeingia matatani na thamani yake kwenye soko kupungua. Kwa
kifupi hayo ndiyo mambo yaliyokuwa yanaisumbua Benki ya Standard hadi
ikabuni mkakati wa kujikwamua.
Mkakati wa Benki ya
Standard ulisukwa kiufundi. Benki iliamua kujishtaki kwa SFO. Mkakati
huu ulilenga kuhamisha kosa kutoka Benki ya Standard Kimataifa na
kutwisha zigo benki zake za Stanbic na Standard zilizoko Tanzania, kwa
madai kwamba maofisa wake wakuu walificha habari, hasa kuhusu shirika
binafsi la kitaaluma la masuala ya fedha (EGMA), ambalo linadaiwa
liliingizwa kinyemela katika mchakato wa Benki ya Standard kutafuta
zabuni na katika majadiliano.
Kutokana na Standard
kujishtaki, matatizo mengi tuliyoyaainisha hapo mwanzoni yametafutiwa
ufumbuzi. Kwanza, mahakama katika uamuzi wake imetamka wazi kwa
kukubaliana kwamba benki hiyo ya kimataifa na wala maofisa wake hawakuwa
na hatia ya kuhusika moja kwa moja katika uvunjaji wa sheria kwa kutoa
rushwa kwa maofsa wa Serikali ya Tanzania ili benki ipate zabuni ya
kuipatia Serikali mkopo huo wa Dola 600 milioni.
Hata
hivyo, mzigo wa nani alitoa rushwa kwa maofsa wa Tanzania zimetupiwa
taasisi za mamlaka nchini Tanzania. Wale maofisa wa Benki ya Standard na
Stanbic Tanzania eti ndiyo wana hatia.
Kwa kiasi
kikubwa ripoti ya Corruption Watch inaibua maswali kuhusu jinsi Benki ya
Standard ilivyotoa habari nusu na zinazojikanganya kuhusu kuhusika
kwake katika mchakato mzima na kwa hakika ni wazi kwamba wale ambao sasa
wanatajwa katika hukumu ya Jaji wa Mahakama ya Uingereza katika kesi ya
Benki ya Standard kujishitaki kwa uvunjifu wa sheria yawezekana kabisa
ni mbuzi wa kafara hasa kwa kuzingatia nani ana mamlaka na kwa lipi
katika biashara hizi kubwa za kimataifa? Je, ni makao makuu au matawi
yake?
Kampuni binafsi ya EGMA ilitoka wapi katika
mchakato? Tanzania kweli imefidiwa ipasavyo kwa uamuzi wa mahakama ya
Uingereza? Haya ni maswali tutakayojibu katika matoleo yajayo ya makala
haya.
0 comments:
Post a Comment