MANISPAA YA KINONDONI KUJENGA KIWANDA CHA TAKA NGUMU SH3.5 BILIONI
Dar es Salaam. Manispaa ya Kinondoni imepewa
Sh3.5 bilioni za kujengea kiwanda cha kuchakata takataka ili kutengeneza
mbolea baada ya meya wake kufanikiwa kuishawishi Halmashauri ya Mji wa
Hamburg nchini Ujerumani.
Kiwanda hicho kitajengwa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza
na wanahabari jana ofisi kwake, meya huyo kutoka Chadema, Boniface
Jacob, ambaye alikuwa pamoja na mwakilishi wa mji wa Hamburg, alisema
maandalizi ya ujenzi wa kiwanda hicho yataanza baada ya mwezi mmoja.
Alisema
kwa siku Kinondoni inazalisha takataka tani 2,026 na zinazopelekwa
dampo ni tani 700, huku 1,326 zikibaki katika maeneo mbalimbali, hivyo
kiwanda hicho kitakuwa kinachukua tani 500 ili kupunguza wingi wa
takataka hizo.
Katika mahojiano na gazeti hili mapema
wiki hii, meya huyo alisema alifanya kazi kubwa ya kuushawishi mji huo
kufadhili mradi huo.
Jacob ambaye pia ni Diwani wa
Ubungo, alisema kiwanda hicho kitakamilika Juni mwakani na kutoa fursa
ya ajira kwa vijana watakaokuwa wakikusanya takataka na wale watakaokuwa
eneo la uzalishaji.
“Baada ya mwezi mmoja tunatarajia
kuanza ujenzi huu. Kinondoni na Humburg ni kama kaka na dada, ndiyo
maana walituambia tutafute ardhi na watasimamia gharama za ujenzi,”
alisema Jacob.
Mwakilishi wa mji huo, Dk Florian
Koelsch alisema halmashauri hiyo ina furaha kutekeleza mradi huo kwenye
Manispaa ya Kinondoni, kutokana na uhusiano mzuri wa muda mrefu uliopo
kati ya halmashauri hizo mbili.
“Malengo yetu ni
mawili; la kwanza ni kupunguza takataka katika manispaa hii, pili ni
kuhakikisha takataka hizi tunazozichukua zinazalisha mbolea
itakayowasaidia wakulima wa Tanzania kuzalisha mazao yao kwa ufanisi,”
alisema Dk Koelsch.
0 comments:
Post a Comment