Monday, November 14, 2016

Sikiliza madudu ya Kocha Mkuu wa Taifa Satrs Baada ya Kupewa kichapo....




Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Charles Boniface Mkwasa amesema timu yake imepoteza kwa bahati mbaya mchezo dhidi ya Zimbabwe huku akitaja magoli mawili ya haraka ya kipindi cha kwanza na kipindi cha pili kuchangia kufanya mchezo kuwa mgumu kwao.
Taifa Stars imepoteza mchezo wake wa kirafiki wa kimataifa kwa kipigo cha magoli 3-0 ugenini dhidi ya wenyeji Zimbabwe.

Tanzania ilisafiri kuelekea mjini Harare ikiwa na nyota wake wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi pamoja na wale wanaocheza ligi ya ndani kucheza mchezo wa kirafiki uliopo kwenye kalenda ya FIFA. Mchezo huo ulikuwa na faida kwa Tanzania kujipandisha kwenye viwango vya FIFA kwama Stars ingepata ushindi.
Kwa upande wa Zimbabwe mchezo huo wameutumia kujipima wakati huu wakijiandaa kucheza fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2017) zinazotarajiwa kufanyika Gabon.

Magoli ya Zimbabwe yamefungwa na Knowledge Musona dakika ya 9, Mathew Rusike dakika ya 55 na Nyasha Mushekwi dakika ya 57.

Stars ilipata nafasi kadhaa za kufunga lakini haikufanikiwa kukwamisha mpira kambani. Mwana Samatta alipata nafasi ya kufunga lakini shuti lake liliokolewa na golikipa wa Zimbabwe kabla ya mpira wa kichwa uliopigwa na Elias Maguli kuokolewa na golikipa huyo aliyecheza kwa kiwango cha juu.
Baada ya mchezo kumalizika, kituo kimoja cha habari kilifanya mazungumzo moja kwa moja na afisa habari wa TFF Alfred Lucas ili kujua kocha wa Taifa Stars Boniface Mkwasa amepokeaje matokeo hayo pamoja na kutaja sababu ya timu yake kupoteza mchezo.

Kwa mujibu wa Alfred Lucas, Mkwasa amesema Stars imepoteza mchezo kwa bahati mbaya lakini aina ya magoli waliyofungwa yaliwachanganya wachezaji.

“Kocha amesema timu imepoteza mchezo kwa bahati mbaya lakini amesema, aina ya magoli yalifyofungwa yaliwachanganya wachezaji na kupelekea kupoteza mchezo. Amesema Zimbabwe ilifunga goli la mapema kipindi cha kwanza (dakika ya 9) ambalo liliwachanganya wachezaji na muda mwingi wakawa wanafikiria zaidi kusawazisha,” amesema Lucas akinukuu maneno ya Mkwasa baada ya mechi.
“Kipindi cha pili wakati Stars ikijipanga kusawazisha, ikafungwa tena goli la mapema (dakika ya 55) na kuvuruga mipango yao ya kuhakikisha wanasawazisha.”

Kwa mujibu wa Alfred Lucas, Stars inatarajia kurejea nchini kesho saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2015 Dar One
| Distributed By Hotrootnews.blogspot.com