UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC,
unapenda kuwataarifa wapenzi wa soka kuwa winga wao Farid Mussa, leo
amepata kibali rasmi cha kufanya kazi nchini Hispania.
Kwa muda mrefu Azam FC imekuwa ikisubiria kibali hicho ili mchezaji
huyo akaanze maisha mapya ya soka nchini humo katika timu ya Deportivo
Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Kufuatia kibali hicho kupatikana, Mussa anatarajia kuondoka nchini muda wowote kuanzia sasa kwenda kuitumikia timu hiyo.
Tunapenda mashabiki wa soka watambue kuwa Mussa anakwenda Tenerife
kwa kwa makubaliano maalumu ya pande zote mbili ukiwa ni usajili wa
mkopo na Azam FC itanufaika kupitia uhamisho wake mwingine
atakaposajiliwa kwenda timu nyingine barani humo.
Tunaamini uwepo wake kwenye klabu hiyo utafanikisha kukuza kipaji
chake zaidi pamoja na thamani yake kwa ujumla, ukizingatia bado ni
mchezaji kijana anayeendelea kujifunza.
Kabla ya kibali hicho kutoka, kuna taarifa mbalimbali zilizotolewa
zikiihusisha Azam FC kuwa tumemzuia kijana wetu huyo kujiunga na timu
hiyo, lakini inaomba ieleweke kuwa kibali kilichotolewa leo hii ndicho
kilichokuwa kikikwamisha uhamisho huo na tunamshukuru Mungu
kimepatikana.
Tunaomba ieleweke kuwa, Azam FC haitafanya jitihada zozote za kuziba
milango ya wachezaji wetu pindi watakapopata timu nje ya nchi, sisi
tutakuwa wa kwanza kuwaongoza katika kufikia malengo yao makubwa ya
kucheza soka la kulipwa kwenye maslahi mazuri endapo taratibu za usajili
zitafuatwa.
Azam FC tunapenda kuishukuru Tenerife kwa kufanikisha uhamisho huo na
tunamtakia mafanikio mema Mussa katika maisha yake mapya ya soka na
tunaamini ataitangaza vilivyo timu yetu kimataifa na Tanzania kwa ujumla
jambo ambalo litafungua milango kwa wachezaji wengine kuungana naye
huko.
Imetolewa na Uongozi wa Azam FC
Jana usiku Azam TV kupitia kipindi cha MSHIKEMSHIKE VIWANJANI
walithibisha kupatikana kwa kibali cha kazi cha kiajana Farid Musa kwa
ajili ya kwenda kucheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Tenerife ya
nchini Hispania, lakini General Manager wa Azam FC Abdul Mohamed
alisikika kwenye radio akithibisha kupokea kibali cha kazi cha winga
huyo ambaye kwa sasa hajacheza mechi yoyote ya kiushindani tangu kuanza
kwa ligi akisubiri safari yake kuelea Ulaya.
Wakala wa Farid Musa, John Sorzano amekanusha habari zilizozagaa kuwa
tayari kibali cha kazi kimeshatoka na badala yake amesema hicho
kilichotapakaa kwenye mitandao ya kijamii si kibali ni form ambayo
itatumiwa katika mchakato wa kuombea kibali.
Solzano ameshangaa form hiyo kutapakaa mitandaoni wakati ni kitu cha
siri huku akisisitiza kuwa, wametumiwa Azam na yeye lakini kwa upande wa
Tanzania, tayari form hiyo imeshaonekana kwenye mitandao ya kijamii.
Kitendo cha hiyo form kusambaa mitandaoni huenda kukahatarisha Farid
kupata kibali cha kazi.
“Hii form nimetumiwa mimi pamoja na klabu ya Azam, lakini nashangaa
wao wameiweka mitandaoni wakati ni kitu cha siri, kwa upande wangu mimi
nilifanya kuwa siri. Farid sio kwamba amepata kibali lakini mchakato
bado unaendelea,” anasema John Sorzano wakala wa Farid Musa.
“Kitendo cha kuitoa form hadharani ambayo ni document ya serikali
kinaweza kikahatarisha mchakato kwasababu ikumbukwe Tanzania pia kuna
ubalozi wa Hispania ambao unaweza kuona yanayofanyika kwenye mitandao ya
kijamii wanaweza wakahoji kwanini document hiyo imesambaa hivyo,
inaweza kuleta ugumu.”